Libasse Gueye, Mngqithi wang’ara Agosti Tuzo TFF
DAR ES SALAAM; Kiungo mshambuliaji wa Simba ya Dar es Salaam, Libasse Gueye, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Agosti wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2026/27, huku Manqoba Mngqithi wa Yanga, akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo. Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi …
DAR ES SALAAM; Kiungo mshambuliaji wa Simba ya Dar es Salaam, Libasse Gueye, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Agosti wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2026/27, huku Manqoba Mngqithi wa Yanga, akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imeeleza kuwa Gueye alitwaa nafasi hiyo baada ya kuonesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Max Nzengeli wa Yanga na Oscar Mwajanga wa Mbeya City, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
“Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitano ambayo Simba ilicheza mwezi huo kushinda yote, huku nyota huyo akifunga bao moja na kuhusika na mengine matano.
“Kwa upande wa Manqoba aliyeingia fainali na Steve Barker wa Simba na Florent Ibenge wa Azam, aliiongoza Yanga kushinda michezo yote mitano iliyocheza mwezi huo na kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi.
“Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Bukombe uliopo mkoani Geita, Deogratius Dayan kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Agosti kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.
“Kamati pia imeteua magoli matatu ambayo yatapigiwa kura na mashabiki ili kupata goli bora la mwezi Agosti. Magoli hayo ni Shekhan Hamis (Singida BS Vs Polisi Tanzania), Robert Mathias (Geita Vs Kagera) na Hija Shamte (Mbeya City v Mashujaa),” imesema taarifa hiyo.