Lamu yageuzwa kambi ya kijeshi wakati wa uzinduzi wa mradi wa Sh2 trilioni
KAUNTI ya Lamu ilikuwa katika ulinzi mkali wa kijeshi jana wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote East Africa Petroleum Refinery kinachotarajiwa kugharimu Sh2 trilioni.
Kuanzia Jeti Kuu ya Mokowe, ambayo ndiyo lango kuu la kuingia Kisiwa cha Lamu, hadi eneo la Kililana katika Bandari ya Lamu ambako hafla hiyo ilifanyika, kulikuwa na uwepo mkubwa wa maafisa wa usalama kutoka vikosi mbalimbali.
Hatua hizo za usalama zilianza kuonekana Jumanne wakati maandalizi ya mwisho ya hafla hiyo yalipokuwa yakiendelea. Maeneo ya Mokowe, Hindi, Mpeketoni, Kisiwa cha Lamu na Bandari ya Lamu yalishuhudia msururu wa maafisa wa usalama waliokuwa wakiratibu operesheni maalum kwa ajili ya kuwapokea viongozi wa mataifa mbalimbali.
Rais William Ruto alikuwa mwenyeji wa hafla hiyo iliyohudhuriwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, viongozi wengine wa Afrika pamoja na bilionea wa Nigeria Aliko Dangote ambaye ndiye mwekezaji mkuu wa mradi huo.
Jana asubuhi, anga ya Kisiwa cha Manda na maeneo ya mradi wa Lapsset ilikuwa na shughuli nyingi za ndege za kijeshi na polisi zilizokuwa zikifanya doria za mara kwa mara. Helikopta hizo zilikuwa zikihakikisha usalama wa viongozi waliokuwa wakiwasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Manda Bay na Uwanja wa Ndege wa Manda.
Baharini pia hali ilikuwa tofauti. Maji ya Bahari Hindi kuanzia Mji wa Lamu hadi Kililana yalikuwa chini ya ulinzi mkali. Meli za Jeshi la Wanamaji la Kenya pamoja na boti za kasi za usalama zilifanya doria mfululizo kuzuia vyombo vya majini visivyoidhinishwa kusogea karibu na eneo la hafla. Meli kubwa ya kijeshi pia ilionekana ikiwa imetia nanga baharini.
Nchini kavu, maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), polisi wa kukabiliana na fujo (GSU) na mashirika mengine ya usalama waliweka vizuizi vya ukaguzi katika barabara kuu zinazoelekea bandari ya Lamu.
Katika lango kuu la kuingia bandarini, wageni wote walilazimika kuthibitisha vitambulisho vyao na kukaguliwa kwa kina kabla ya kuruhusiwa kuingia.
Licha ya hatua hizo kali za usalama, hali ndani ya eneo la hafla ilikuwa ya shangwe huku viongozi wa jamii, vijana na wageni kutoka ndani na nje ya nchi wakikusanyika kushuhudia uzinduzi wa mradi huo mkubwa.
Hali ya usafiri wa anga pia ilikuwa ya kipekee huku helikopta zikifika mfululizo bandarini zikibeba viongozi na wajumbe mbalimbali.
Saa sita na dakika ishirini na mbili mchana, Rais Ruto akiwa pamoja na Rais Museveni na Waziri Mkuu Abiy Ahmed walishika koleo na kuchota udongo kuashiria kuanza rasmi kwa ujenzi wa mradi huo.
Muda mfupi baadaye, ndege za kijeshi za KDF zilifanya maonyesho maalum angani kuonyesha kuwa eneo hilo lilikuwa salama kwa uwekezaji mkubwa wa kimkakati kama huo.
Katika hotuba yake, Bw Dangote alifichua baadhi ya matukio yaliyotokea wakati Rais Ruto na mkewe Rachel Ruto walipotembelea kiwanda chake cha kusafisha mafuta mjini Lagos, Nigeria. Alisema Mama wa Taifa alionyesha hamu kubwa ya kujifunza kuhusu mchakato wa usindikaji wa mafuta kiasi kwamba alionekana kama mwanafunzi wa uhandisi wa kemikali.
Dangote pia alimpongeza Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo kwa mchango wake katika miradi yake ya awali ya viwanda nchini Nigeria.
Wakati huo huo, wafanyabiashara wa Lamu walinufaika pakubwa kutokana na hafla hiyo. Hoteli nyingi zilijaa wageni huku biashara za mikahawa, vituo vya mafuta, usafiri na huduma nyingine zikirekodi ongezeko kubwa la wateja.