Kocha Gaborone: Presha yote ipo Yanga
DAR ES SALAAM: KOCHA wa Gaborone United ya Botswana, Sean Connor, amesema presha kubwa ipo kwa Yanga kuelekea mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, akisema wenyeji watakuwa na mzigo wa kucheza mbele ya mashabiki wao. Yanga itakuwa mwenyeji wa Gaborone United kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, katika mchezo ambao una umuhimu …
DAR ES SALAAM: KOCHA wa Gaborone United ya Botswana, Sean Connor, amesema presha kubwa ipo kwa Yanga kuelekea mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, akisema wenyeji watakuwa na mzigo wa kucheza mbele ya mashabiki wao.
Yanga itakuwa mwenyeji wa Gaborone United kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, katika mchezo ambao una umuhimu mkubwa kwa timu zote mbili katika harakati za kusonga mbele katika mashindano hayo.
Connor amesema anatarajia mchezo mgumu na wa kuvutia kutokana na ubora wa timu zote mbili, lakini anaamini Gaborone United ina uwezo wa kupata matokeo mazuri.
“Nadhani presha kubwa ipo upande wa Yanga kuliko sisi. Huu ni mchezo wao wa nyumbani, watakuwa na mashabiki wengi na pia vyombo vingi vya habari. Kwa hiyo presha yote ipo upande wao. Ni moja ya klabu kubwa Tanzania, lakini sisi ni klabu kubwa zaidi Botswana, hivyo tunajiamini,” amesema.
Connor amesema wamebaini maeneo ambayo wanaamini wanaweza kuitumia Yanga, ingawa hakutaka kuweka wazi udhaifu huo kabla ya mchezo.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema timu yake imejipanga kufanya vizuri, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia nafasi zitakazozalishwa na kuwa makini katika kuzuia mipira mirefu ya wapinzani.
Mngqithi amesema anatarajia kuona Yanga ikifanya vizuri katika mchezo huo na kutumia vizuri nafasi itakazopata ili kupata mabao.
“Tumekuwa tukizalisha nafasi nyingi, lakini bado sifurahishwi na aina ya nafasi ambazo tumekuwa tukizitengeneza. Ninaamini utakuwa mchezo ambao nafasi zote tutakazozalisha tutazitumia vizuri na zitaleta mabao mengi kwetu,” amesema Mngqithi.
Amesema Gaborone United ni timu nzuri katika kutumia nafasi na mipira mirefu, hivyo Yanga inapaswa kuwa makini ili isiruhusu wapinzani kupata nafasi za kuitia kwenye matatizo.