Kamati yapongeza polisi kuimarisha usalama
DODOMA: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Jijini Dodoma leo. Ayoub amesema wizara inaendelea kuimarisha amani na usalama wa raia pamoja na mali zao. Amebainisha …
DODOMA: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Jijini Dodoma leo.
Ayoub amesema wizara inaendelea kuimarisha amani na usalama wa raia pamoja na mali zao.
Amebainisha kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kufanya doria, misako na operesheni katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ulinzi shirikishi.
Aidha, amesema wizara kupitia Jeshi la Polisi imendelea kuimarisha usalama barabarani kupitia ukaguzi wa vyombo vya moto, mafunzo kwa madereva na matumizi ya teknolojia ikiwemo Global Positioning System (GPS) na kamera za usalama barabarani katika maeneo muhimu ili kufuatilia mienendo ya Madereva na Wanaokiuka Sheria za barabarani.
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa mtandaoni kupitia matumizi ya vifaa vya kisasa, mafunzo kwa watendaji na matumizi ya teknolojia ili kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Najma Murtaza Giga akizungumza kwa niaba ya Kamati amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa linayofanya katika kulinda amani na usalama wa wananchi.
Amesema wananchi bado wana imani na Jeshi hilo na wanatambua kazi kubwa inayofanywa na Jeshi hilo katika kuhakikisha wanachi wanaendelea kuishi kwa amani huku akieleza kuwa changamoto zinazojitokeza haziwezi kutatuliwa na Jeshi la Polisi pekee bali kwa ushirikiano na wadau mbalimbali
Kadhalika, amesema Kamati iko tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi pale watakapohitaji jambo lolote linalohitaji msukumo wa Kamati hiyo.
Aidha, amemshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, Naibu Waziri pamoja na Viongozi wa Wizara hiyo kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya.