Iringa yajipanga matumizi mbegu bora

Habari Leo
Published: Aug 24, 2026 17:16:12 EAT   |  News

IRINGA: WAKULIMA mkoani Iringa wamehimizwa kutumia mbegu bora na zilizoidhinishwa ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao, huku Serikali ikiimarisha mikakati ya kudhibiti mbegu bandia na kuwawezesha wakulima kupata pembejeo zenye ubora kwa wakati. Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kuongeza uzalishaji wa kilimo mkoani humo, hasa wakati wakulima wakijiandaa kwa msimu mwingine …

IRINGA: WAKULIMA mkoani Iringa wamehimizwa kutumia mbegu bora na zilizoidhinishwa ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao, huku Serikali ikiimarisha mikakati ya kudhibiti mbegu bandia na kuwawezesha wakulima kupata pembejeo zenye ubora kwa wakati.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kuongeza uzalishaji wa kilimo mkoani humo, hasa wakati wakulima wakijiandaa kwa msimu mwingine wa kilimo, kwa kuzingatia umuhimu wa kuanza maandalizi mapema na kutumia mbegu zinazoendana na mazingira ya kilimo ya maeneo yao.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Magozi, Kata ya Ilolo Mpya, Wakala Mkuu wa Mbegu za Serikali (ASA) chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mgongolwa Agrovet and Seeds, Joseph Mgongolwa, ameipongeza serikali kwa kuendelea kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora za ruzuku huku ikiimarisha elimu ya kuzitambua na kuzitumia kwa usahihi.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwakinga wakulima dhidi ya wafanyabiashara wanaouza mbegu zisizo na ubora, ambazo zinaweza kusababisha hasara kwa wakulima kutokana na kushuka kwa kiwango cha uotaji na uzalishaji.

Aidha Mgongolwa amepongeza mpango wa uwepo wa mawakala katika maeneo mbalimbali akisema utasaidia kurahisisha upatikanaji wa mbegu zilizoidhinishwa na kupunguza mianya ya wafanyabiashara wanaoweza kutumia fursa hiyo kuuza mbegu bandia.

Amesema matumizi ya mbegu bora, yakichanganywa na kanuni bora za kilimo, yana nafasi kubwa katika kuongeza tija kwa mkulima na hatimaye kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Kata ya Ilolo Mpya, Oswald Kapungu, amewataka wakulima kutumia ushauri wa wataalamu wa kilimo katika kuchagua mbegu kulingana na aina ya zao, eneo na mazingira ya kilimo.

Amesema wakulima wanapaswa pia kuzingatia maandalizi ya mashamba, muda sahihi wa kupanda na matumizi sahihi ya pembejeo ili kuhakikisha mbegu bora zinatoa matokeo yanayotarajiwa.

Naye Diwani wa Kata hiyo, Patrick Muhegele, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kusikiliza changamoto za wakulima kwa kuhakikisha wanapata mbegu bora kwa gharama nafuu, akiwataka kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji.

Muhegele amewataka wakulima kuanza maandalizi ya mashamba mapema na kuhakikisha wanapata mbegu kwa wakati ili kuepuka kuchelewa kuanza msimu wa kilimo.

Baadhi ya wakulima wa Kijiji cha Magozi wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mbegu bora za ruzuku, wakisema hatua hiyo imeongeza matumaini ya kuongeza uzalishaji na kipato kupitia kilimo.

Hata hivyo, wameiomba Serikali kuendelea kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao yao ili ongezeko la uzalishaji liendane na fursa za kuuza mazao kwa bei nzuri.