Iringa yajiandaa usiku wa miujiza na sauti za mbinguni

Iringa inatarajia kushuhudia mwamko mpya wa kiroho Disemba 19 mwaka huu, wakati timu ya The Light Worship Team itakapoandaa tamasha kubwa la kusifu na kuabudu lijulikanalo kama “Maskani Worship Gathering – Ni Shwari”, litakalofanyika katika ukumbi wa Sambala. Tamasha hilo linatarajiwa kuwa zaidi ya tukio la muziki wa injili — ni mwaliko wa kipekee wa …
The post Iringa yajiandaa usiku wa miujiza na sauti za mbinguni first appeared on HabariLeo.
Iringa inatarajia kushuhudia mwamko mpya wa kiroho Disemba 19 mwaka huu, wakati timu ya The Light Worship Team itakapoandaa tamasha kubwa la kusifu na kuabudu lijulikanalo kama “Maskani Worship Gathering – Ni Shwari”, litakalofanyika katika ukumbi wa Sambala.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwa zaidi ya tukio la muziki wa injili — ni mwaliko wa kipekee wa kuwaleta watu karibu na Mungu, kurejesha matumaini na kuibua ari mpya ya kiroho kwa wakazi wa Iringa na maeneo ya jirani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwimbaji na Mtumishi wa Mungu, Ombeni Stony, ambaye pia ni kiongozi wa The Light, alisema tamasha hilo limebeba ujumbe mzito wa amani, upendo na urejeo kwa Mungu.
“Maskani ni mahali pa utulivu. Tunataka kila mtu atambue kuwa kwa Mungu hakuna linaloshindikana. Huu ni wakati wa watu kukaa chini ya uwepo wa Mungu, wasikilize sauti yake, na kubadilishwa,” alisema Stony kwa msisitizo.
Alisema pamoja na kusifu na kuabudu, kutakuwa na matukio maalum ya kiroho yatakayogusa maisha ya watu — ikiwemo maombezi, mafundisho ya imani, na nafasi za kutoa sadaka kwa moyo wa hiari.
Hata hivyo, kuingia ni bure, na tiketi maalum zitatolewa kwa utaratibu wa kutoa sadaka.
Stony alibainisha kuwa Maskani Worship Gathering ni mwendelezo wa matukio ya kiroho yaliyoanzishwa na The Light miaka iliyopita kama Maskani Jogging na programu nyingine za uinjilisti, zenye lengo la kukuza ibada zenye uhai na zinazoleta mabadiliko ya ndani.
Kwa upande wake, Mlezi wa The Light, Dk Jesca Msambatavangu, alisema tamasha hilo linawahusu watu wa rika zote, likiwa jukwaa la familia, vijana na wazee kujumuika katika uwepo wa Mungu.
“Mambo ya dunia yanapita, lakini mambo ya Mungu hayapiti. Tunawakaribisha watu wote – kama familia, marafiki au mtu binafsi – waje Sambala tarehe 19. Hapa ni mahali pa kufutiwa huzuni, kufarijiwa na kujazwa tena nguvu ya kiroho,” alisema.
Aidha, Msambatavangu aliwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi, hasa wale waliopoteza matumaini katika maisha ya ndoa, kazi au huduma, akisema watapata faraja, mafunzo na fursa ya kukutana na Mungu anaebadili maisha.
Naye Amenye Kalinga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa The Light, alisema tamasha hilo litapambwa na waimbaji mahiri akiwemo Clement Paul, Donick Mwakatobe, Victor Maestro, na mwenyeji Ombeni Stony.
“Tunataka watu waone tofauti – si tamasha la burudani, bali ni ibada hai ya kipekee. Ni usiku wa miujiza na sauti za mbinguni zitakazogusa roho za watu,” alisema Kalinga.
Tamasha hili limebeba kauli mbiu “Ni Shwari”, ikikumbusha kuwa katika uwepo wa Mungu kuna amani, matumaini na nguvu mpya za kuanza upya.
The post Iringa yajiandaa usiku wa miujiza na sauti za mbinguni first appeared on HabariLeo.