IEBC, NCIC na Polisi watoa tahadhari kuhusu dalili za hatari uchaguzi mkuu ujao
KENYA inapoelekea uchaguzi mkuu wa 2027, tayari kuna ishara za hatari zinazoweza kuzua vurugu na kuzamisha nchi katika mzozo wa kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Vurugu katika mikutano ya kisiasa, matamshi ya chuki, madai ya wizi wa kura, mizozo kuhusu zabuni za mabilioni ya fedha, taarifa za uongo na kupungua kwa imani kwa taasisi za uchaguzi ni baadhi ya changamoto zinazotajwa.
Masuala hayo yalijadiliwa jana katika mkutano wa kitaifa wa usalama wa uchaguzi uliofanyika Nairobi.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) na Idara ya Mahakama zilitahadharisha kuhusu umuhimu wa kujifunza kutokana na machungu ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/08.
Ghasia hizo zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,100, 3,500 kujeruhiwa na hadi 600,000 kuhama makazi yao.
Ripoti ya Kofi Annan Foundation ya Electoral Vulnerability Index ya 2026–2027 iliyotolewa Julai ilianika uwezekano wa Kenya kukumbwa na aina fulani ya ghasia zinazohusiana na uchaguzi kuwa asilimia 81.6.
Ripoti hiyo ilitaja ukosefu wa imani kwa IEBC, ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira kwa vijana, siasa za ukabila na wasiwasi kuhusu mwenendo wa polisi wakati wa maandamano.
Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alisema tume hiyo imekuwa ikielekezewa na madai mazito kutoka kwa viongozi wa kisiasa kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa 2027.
Alisema madai yasiyothibitishwa yanaweza kudhoofisha imani ya wananchi katika IEBC kabla kampeni hazijaanza kikamilifu.
“Tunahitaji kuchunguza ukweli kuhusu baadhi ya madai haya ya ajabu ambayo yanalenga kuwafanya Wakenya waamini kwamba uchaguzi hautakuwa huru na wa haki,” alisema.
Kauli yake ilijiri baada ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kudai IEBC inapanga kuiba uchaguzi wa 2027 kupitia mfumo mpya wa usimamizi wa uchaguzi.
Pia kuna mzozo kuhusu zabuni ya mabilioni ya fedha ya mfumo wa teknolojia utakaotumiwa katika uchaguzi huo.
Bw Ethekon alisema IEBC italinda uhuru wake na kupinga juhudi zozote za kudhoofisha uaminifu kwa tume.
Alisema hata hivyo IEBC haiwezi kufanikisha uchaguzi wa kuaminika bila ushirikiano wa polisi, mahakama na taasisi nyingine.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga alionya kuwa uchunguzi dhaifu na ukosefu wa ushahidi unatatiza juhudi za kuwafungulia mashtaka wahusika wa vurugu za kisiasa na uchochezi.
Aliwataka polisi na DCI kukusanya ushahidi unaohusisha washukiwa na uhalifu, wakiwemo wale wanaofadhili au kupanga makundi ya vijana wanaotumika kuvuruga mikutano.
Alisema kuwakamata vijana pekee bila kuwafuatilia wanaowafadhili hakutamaliza tatizo.
Mwenyekiti wa NCIC, Askofu Kepha Omae, alisema tume hiyo ina wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa matamshi ya chuki na uchochezi kadiri shughuli za kisiasa zinavyozidi.
Alisema NCIC itachukua hatua dhidi ya wanasiasa na Wakenya wengine wanaokiuka sheria kupitia kauli zao.
Tume hiyo pia imekuwa ikifuatilia jumbe zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ikiwemo WhatsApp na TikTok.
Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alisema Polisi wameanza kutekeleza mpango wa usalama wa uchaguzi wa 2027.
Jaji Daniel Musinga, aliyekuwa mgeni rasmi, alisema vitisho vipya kama matamshi ya chuki, taarifa za kupotosha, propaganda za kisiasa na matumizi ya teknolojia kuwanyanyasa wanawake kisiasa vinahitaji taasisi mbalimbali kushirikiana.