Hisa wanazomiliki Waatanzania kampuni migodini kuchunguzwa

Habari Leo
Published: Oct 02, 2026 13:59:03 EAT   |  Business

GEITA; Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameiagiza Tume ya Madini kufanya uchunguzi uhalali wa hisa wanazomiliki Watanzania katika kampuni za kigeni zinazotoa huduma migodini. Mavunde ameiagiza uchunghuzi huo ufanyike kwa kushirikisha mamlaka zinazohusika, ikiwemo Wakala wa Usajili (BRELA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Mavunde ametoa maagizo hayo katika kongamano la Ushirikishwaji Watanzania kupitia Kanuni …

GEITA; Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameiagiza Tume ya Madini kufanya uchunguzi uhalali wa hisa wanazomiliki Watanzania katika kampuni za kigeni zinazotoa huduma migodini.

Mavunde ameiagiza uchunghuzi huo ufanyike kwa kushirikisha mamlaka zinazohusika, ikiwemo Wakala wa Usajili (BRELA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mavunde ametoa maagizo hayo katika kongamano la Ushirikishwaji Watanzania kupitia Kanuni ya 13A kwenye Viwanja vya Maoneesho ya Teknolojia ya Madini Manispaa ya Geita.

Amesema kifungu cha 133 na kifungu cha 135 cha sheria ya madini sura ya 133 kimetoa mashariti ya lazima kwa kila mmiliki wa leseni kuhakikisha anatumia bidhaa na huduma za Tanzania.

“Kama huduma hiyo haipatikani hapa Tanzania akimpata mtu wa nje ahakikishe huyo mtu wa nje anaingia makubaliano ya ubi ana Mtanzania awe na umiliki wa hisa usiopungua asilimia 20,” amesema.

Amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha Watanzania wanashiriki moja kwa moja kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya madini kupitia biashara na huduma mbalimbali.

Amesema pamoja na uzuri wa sheria hiyo wamejitokeza watu kughushi umiliki wa hisa za kampuni za utoaji wa huduma kwenye kampuni za uchimbaji migodini.

Amesema taarifa ya awali imebaini baadhi ya wawekezaji kughushi nyaraka ama kuwamilikisha watanzania asilimia 20 ya hisa hewa za kampuni jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Tunataka tuondoe janja janja yote ili sekta hii ibaki kuwa sekta imara na yenye kuaminika na Watanzania wanufaike,”, amesema Mavunde.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti amesema ipo haja ya kuchukua hatua za haraka kufuatilia Watanzania wanaoshiriki kughushi umiliki wa hisa kwani inaminya fursa za Watanzania.