Hifadhi ya Saadani na maajabu sanamu ya Bikira Maria

PWANI; Sanamu ya Bikira Maria (Mariam), anayesemwa katika vitabu vitakatifu vya Biblia Takatifu na Kurani Tukufu kuwa ni Mama wa Yesu Kristo (Issa bin Mariam), iliyogundulika ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani inatajwa kuwa maajabu mapya yasiyo ya kawaida kwa macho na masikio ya watalii ndani na nje ya Tanzania huku ikiongeza upekee wa …
PWANI; Sanamu ya Bikira Maria (Mariam), anayesemwa katika vitabu vitakatifu vya Biblia Takatifu na Kurani Tukufu kuwa ni Mama wa Yesu Kristo (Issa bin Mariam), iliyogundulika ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani inatajwa kuwa maajabu mapya yasiyo ya kawaida kwa macho na masikio ya watalii ndani na nje ya Tanzania huku ikiongeza upekee wa hifadhi hiyo kiutalii.
Akizungumza akiwa ndani ya eneo la hifadhi, Ofisa Mhifadhi katika Utalii, Hifadhi ya Taifa Saadani (SANAPA), Daud Gordon anasema kivutio hicho kipya kinaweza kufaa kutumika kama nyenzo muhimu kukuza utalii wa kiimani na hata kuwa sehemu ya hija kwa waamini, hasa wanaoamini na kumheshimu Mama huyo kadiri ya mapokeo ya imani zao.
Anasema sanamu hiyo inaweza kuwapa wageni fursa ya kutafakari juu ya ukuu wa Mungu, uumbaji wake na imani wanazozishikilia huku wakiwa katikati ya maajabu ya asili.
“Hili ni jambo la kipekee, si hadithi bali ni uhalisia. Sanamu hiyo, ambayo inaonekana ndani ya mti wa mbuyu, imeshuhudiwa na watalii mbalimbali wanaofika hapa, nanyi wanahabari mliotembelea hifadhi yetu,” anasema Gordon.
Anaongeza: “Sanamu hiyo ipo ndani ya Hifadhi ya Saadani inayopatikana katika mikoa ya Pwani (Wilaya ya Bagamoyo) na Tanga (Wilaya ya Pangani) ikiwa hifadhi pekee nchini inayopakana moja kwa moja na Bahari ya Hindi.”
Gordon ambaye pia Ofisa Mhifadhi anayesimamia Kitengo cha Utalii, anasema watalii wa ndani na nje wameanza kutembelea sanamu hiyo, huku akihimiza na kualika watalii zaidi hasa wa ndani kufika na kujionea maajabu hayo pamoja vivutio vingine ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani.
Kwa mujibu wa Mwongoza Watalii katika eneo hilo, Fredy Nesto sanamu hiyo iligundulika mwaka 2019 ikiwa katika mbuyu wenye zaidi ya miaka 100 na ambao historia inaonesha kwa kipindi fulani, wakoloni waliutumia kunyongea watumwa.
“Sanamu hiyo ya Bikira Maria inaonekana vizuri zaidi mtu akiwa umbali wa wastani, lakini ukiwa karibu inapotea, hayo pia ni majabu ya sanamu hiyo,” anasema Nesto.
Kwamba, tayari watalii kutoka maeneo mbalimbali wameanza kufika eneo hilo na kuitumia kwa maombi kwa shida mbalimbali walizo nazo, baadhi wakirudi kueleza maombi waliyofanya katika eneo hilo yalivyofanikisha kuondoa shida zao.
Akielezea upekee wa Hifadhi ya Taifa Saadani, Gordon anasema: “Upekee wake hauishii tu kwenye mandhari ya kuvutia ya pwani, bali pia kwa wanyamapori kama simba, tembo na pundamilia ambao huonekana vizuri na kwa ukaribu zaidi wakifika ufukweni kupumzika, jambo ambalo ni adimu duniani.”
Anasema hifadhi hiyo pia ina mazalia ya kasa wa baharini ambao huvutwa na mazingira ya hifadhi wakati wa msimu wa kuzaliana kutoka maeneo mbalimbali ya bahari duniani.
Gordon anataja mchanganyiko wa maji kati ya Mto Pangani na Bahari ya Hindi kuwa unaongeza uzuri wa kiasili wa hifadhi hiyo, sambamba na uwepo wa aina nne kati ya tano za wanyama wakubwa wa Afrika ambao ni tembo, simba, twiga na nyati. Wanyama wanaokosekana kati ya watano hao ni faru pekee.
Anasema hayo yote kwa pamoja yanaifanya Hifadhi ya Taifa Saadani kuwa ya kipekee nchini Tanzania na barani Afrika.
Upekee vivutio Hifadhi ya Saadani
Licha ya Tanzania kuwa na hifadhi za taifa 21 zenye vivutio mbalimbali vya utalii, Hifadhi ya Taifa ya Saadani imebahatika kuwa na vivutio vya kipekee barani Afrika hivyo kuitofautisha na nyingine.
Kimsingi yapo mambo manne yanaelezwa kuitofautisha na hifadhi nyingine nchini na barani Afrika, hivyo kuifanya kuwa ya kipekee. Ina ukubwa wa takribani kilomete za mraba 1,100.
Anataja mambo hayo kuwa ni makutano ya bahari na nyika, uwepo wa mlango bahari wa Mto Wami unaoingia Bahari ya Hindi, mazalia ya kasa wa kijani pamoja na wanyama na binadamu kukutana kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi wakivinjari na kuifanya ya pekee zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Kimsingi, hilo haliishii kwenye mandhari ya kuvutia tu, bali pia makundi ya wanyama zaidi ya matano wenye hadhi ya juu kama simba, tembo na pundamilia ambao hufika ufukweni kupumzika; jambo ambalo ni adimu katika hifadhi nyingine duniani.
Inaelezwa pia kuwa, Hifadhi ya Saadani inao Msitu wa Zalaninge ambao una uoto wa asili kabisa unaochangia upatikanaji wa mvua pamoja na miti ya mikoko inayosaidia viumbe hai kama kasa kuzaliana kwa wingi katika eneo hilo.
Anasema: “Saadani tunashughulika na utalii wa aina mbalimbali ikiwa na pamoja na utalii wa kutembea kwa miguu, kuangalia wanyama mchana na usiku, utalii wa kwenye maji katika Mto Wami ambao pia una eneo la makutano na Bahari ya Hindi lakini maji yake hayachanganyiki.
“Hifadhi hii ina utalii wa aina nyingi, pia tunasimamia Kituo cha malikale chenye kumbukumbu ya biashara ya utumwa cha Caravan Serai cha mjini Bagamoyo, eneo la magofu yaliyotumika kuhifadhi watumwa, mbuyu uliotumika kunyongea watumwa na makaburi ya wamisionari waliokuja kueneza dini katika ene hili la Pwani,” anasema.
Anaongeza: “Tunao pia utalii wa dini, tuna eneo la mti wa mbuyu ambao una nembo ya sanamu ya Bikira Maria, huenda ni kumbukizi, ni asili ambayo hakuna aliyeichora bali imekutwa hapo, huu ndiyo upekee wa Saadani…”
Ofisa mhifadhi huyo katika Kitengo cha Utalii, anasema ili kuendelea kuimarisha hifadhi hiyo, wametenga maeneo tisa kwa ajili ya uwekezaji upande wa huduma za malazi, utalii wa fukwe na michezo ya baharini.
Anasema hifadhi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2005 kutoka kuwa pori la akiba ina malango makuu ya nchi kama Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius (JNIA), Bandari Kuu, miji ya kihistoria ya Bagamoyo na Zanzbar na kufanya kufikika kwa urahisi ikitumia usafiri wa anga, maji na barabara kwani panafikika kwa njia ya maji, gari na ndege kwa kuwa kuna uwanja wa ndega unaoweza kutua ndege ndogo, karibu zaidi na Dar es Salaam na Zanzibar.
Aidha, kuna magofu ya soko la kale la watumwa, bandari ya kale iliyotumika kusafirisha watumwa, mbuyu uliotumika kunyongea watumwa wakorofi na dhaifu na makaburi ya wapelelezi wa Ujerumani wa kwanza kuingiza Ukristo Saadani.
Mmoja wa viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Alei Levorosi, Arusha Mjini, Lucas Mollel anasema mambo mbalimbali aliyoyaona kwenye Hifadhi ya Saadani yamemwimarisha zaidi kiimani kwani ameshuhudia uumbaji wa Mungu usio wa kawaida.
“Tuna kila saabu ya kumshukuru Mungu, sijawahi kuona maji yapo karibu na bahari ambayo hayana chumvi, haya ni maajabu, nimeona vifaa vilivyotumika kufunga watumwa. Niwaombe sana taasisi za dini na za Serikali kuwaleta viongozi wao kuja hapa kupumzisha akili na kujifunza mambo ya kale, kutafakari ukuu wa Mungu,” anasema Mollel.
Mwandishi ni msomaji wa gazeti hili. Kitaaluma ni mwandishi wa habari.