Gugu karoti tishio kwa ikolojia, wanyamapori

Habari Leo
Published: Jun 06, 2025 08:53:23 EAT   |  Travel

“GUGU Karoti ni tishio kwa uoto wa asili, malisho ya mifugo na maisha ya wanyamapori. Kwa msingi huo, ushirikiano wa jamii ni silaha kuu dhidi ya mmea huu vamizi.” Ofisa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Gregory Mtega anasema hayo wakati akitoa elimu kwa wananchi wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha …

“GUGU Karoti ni tishio kwa uoto wa asili, malisho ya mifugo na maisha ya wanyamapori. Kwa msingi huo, ushirikiano wa jamii ni silaha kuu dhidi ya mmea huu vamizi.”

Ofisa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Gregory Mtega anasema hayo wakati akitoa elimu kwa wananchi wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha kuhusu namna ya kukabiliana na mmea huo hatarishi.

Mmea vamizi unaojulikana kama gugu karoti umeendelea kuleta changamoto kubwa kwa uoto wa asili, malisho ya mifugo na maisha ya wanyamapori katika maeneo ya hifadhi na vijiji hali inayoibua haja kubwa ya ushirikiano wa dhati kati ya jamii na mamlaka za uhifadhi.

Mmea huo umeenea kwa kasi katika baadhi ya maeneo ya ushoroba wa Upper Kitete unaounganisha Hifadhi ya Ngorongoro, Ziwa Manyara na Tarangire. Gugu karoti huzaliana kwa kiwango kikubwa cha zaidi ya mbegu 40,000 kutoka mmea mmoja hali inayotishia mifumo ya ikolojia.

Kwa mujibu wa Mtega, NCAA imedhamiria kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi shirikishi, kugawa miche ya miti, mizinga ya nyuki na kushirikiana na wananchi kung’oa mimea vamizi ili kuimarisha malisho, kuboresha mazingira na kukuza uhifadhi endelevu.

Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Kornelio Lengai anasema mmea huo umekuwa chanzo cha kushuka kwa uzalishaji wa chakula na upatikanaji wa malisho, hivyo juhudi za pamoja kuukabili zinahitajika. “Unakuta mashamba yanakauka, mifugo inakosa malisho na jamii inaathirika moja kwa moja. Hii ni changamoto inayohitaji mikakati endelevu na ushirikiano wa wadau wote,” anasema Lengai.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), asili ya gugu karoti ni Amerika ya Kati na Kusini, lakini kwa sasa limeenea kwa kasi katika nchi kadhaa za Afrika ikiwemo Tanzania. Kimsingi, mmea huo huharibu ardhi kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupunguza rutuba na kusababisha matatizo ya kiafya kwa binadamu na wanyama.

Taarifa ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuhusu utafiti uliofanyika Simanjiro inaonesha mmea huo huzuia ukuaji wa mimea mingine kwa kutoa kemikali za sumu na hivyo, kutishia uhai wa bayoanuwai, mifugo na hata usalama wa chakula.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Costech inapendekeza matumizi ya njia za kibaiolojia kama vile uzalishwaji wa wadudu maalumu wanaokula au kuzuia mmea huo, sambamba na upandaji wa mimea ya asili inayokinzana na gugu karoti.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana anasema serikali imeanzisha mpango wa kitaifa wa kudhibiti mimea vamizi ikiwa ni pamoja na kutumia nyuki kama njia rafiki ya mazingira kuzuia ueneaji wa mmea huo.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Mazao Tanzania (TARI), njia hiyo ya kibaiolojia imefanikiwa katika nchi kama India na Australia na kwamba, ni muhimu kwa serikali kushirikiana na watafiti kuzalisha wadudu maalumu wanaoweza kudhibiti mmea huo bila kuathiri viumbe wengine.

TARI inaelekeza jamii kupanda mimea shindani itakayosaidia kukwamisha ukuaji wa mmea huo kwa kuwa matumizi ya mimea ya asili yenye uwezo wa kushindana na kuzuia ueneaji wa gugu karoti ni nyasi za malisho ambazo huchangia kuimarisha malisho kwa mifugo huku yakikandamiza ukuaji wa mmea huo.

Tari pia inasisitiza uwepo wa sera na kibali maalumu cha kuingiza au kuachilia wadudu wa kudhibiti mimea vamizi kwa kuzingatia taratibu za kisayansi na kisheria. Kwamba, hilo litafanikiwa kwa ushirikiano mkubwa baina ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na tathmini ya athari kwa mazingira kuhakikisha hakuna madhara ya muda mrefu.

Aidha, utafiti uliofanywa na Leticia Musese kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ukilenga kuchunguza athari za gugu karoti kwenye utofauti wa mimea asilia maeneo ya Simanjiro nao utatumika katika kazi hiyo ya kutokomeza mimea vamizi hiyo.

Matokeo yanaonesha kuwa, uwepo wa gugu karoti ulipunguza kwa kiasi kikubwa tofauti ya mimea asilia na hivyo kuathiri upatikanaji wa malisho kwa mifugo na wanyamapori. Utafiti huo unabainisha uhusiano kati ya uwepo wa gugu karoti na mabadiliko katika upatikanaji wa malisho kwa wanyama huku kukiwa na mabadiliko ya kiikolojia yatokanayo na ueneaji wa mmea huo.

“Maeneo yenye gugu karoti yalikuwa na idadi ndogo zaidi ya aina za mimea ikilinganishwa na yale ambayo hayajaathirika, maeneo yaliyoathirika yalikuwa na aina 12 hadi 15 za mimea huku yasiyoathirika yakiwa 25 hadi 30 za mimea, hivyo kupungua kwa zaidi ya asilimia 50 katika utofauti wa mimea,” unaeleza utafiti huo.

Mkazi wa Kijiji cha Upper Kitete, Emmanuel Siriri anasema juhudi za kung’oa mmea huo zimefungua fursa mpya za ajira kwa vijana na kurejesha hali nzuri ya kilimo. “Bado kuna changamoto ya upatikanaji wa rasilimali na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendeleza ueneaji wa mmea huu,” anasema.

Gugu karoti limekuwa mfano halisi wa namna changamoto za mazingira zinavyoweza kutatuliwa kupitia ushirikiano wa jamii, watafiti na serikali. Wadau mbalimbali wanasema bila mikakati ya pamoja na hatua mbalimbali madhubuti kuchukulia, mimea hiyo inaweza kuendelea kudhoofisha maisha, uchumi na bayoanuai ya taifa.