GHANA imetangaza kuwa inaunga mkono mpango wa Morocco wa kusimamia Western Sahara lakini ifanye hivyo kwa kufuata mwongozo uliowekwa na Umoja wa Kitaifa (UN).
Algeria imekuwa ikiunga mkono wapiganaji wa Polisario front kusimamia Western Sahara na pia ikisukuma eneo hilo litambuliwe kama nchi kivyake.
Morocco na Algeria zimekuwa na uhasama mkubwa wa kidiplomasia kila mmoja wao akisukuma kuwa na ushawishi kuhusu jinsi Western Sahara itakavyoongozwa na kudhibiti.
Hatua ya Ghana sasa inaiongeza kwenye orodha ya nchi kutoka Ulaya, Afrika na Uarabuni ambazo zinaunga mkono Morocco itanue mawanda yake ya uongozi hadi Western Sahara.
“Ghana inaunga mkono Morocco katika mpango wake wa kusimamia Western Sahara. Ni vyema kuwa mzozo huu ambao umedumu kwa kipindi kirefu pia upate suluhu,” ikasema taarifa ya pamoja ya Ghana na Morocco.
Taarifa hiyo ilitolewa baada ya mkutano kati ya Waziri wa Masuala ya Nje wa Ghana Samuel Ablakwa na mwenzake wa Morocco Nasser Bourita jijini Rabat.
“Umoja wa Kitaifa unasalia jukwaa pekee ya kupata suluhu kuhusu suala hili,” ikaongeza taarifa hiyo.
Kenya na Uingereza siku chache zilizopita pia zilisema zinaunga mkono Morocco kusimamia Western Sahara.