GGML yajipanga afya ya uzazi shuleni

GEITA; KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imeanza utekelezaji wa mpango wezeshi kufanikisha mazingira rafiki ya afya ya uzazi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Geita. Mpango huo unatekelezwa kupitia mradi wa usambazaji wa taulo za kike kwa wanafunzi waweze kujisitiri wakati wa hedhi pamoja na ufadhili wa mafunzo ya …
GEITA; KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imeanza utekelezaji wa mpango wezeshi kufanikisha mazingira rafiki ya afya ya uzazi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Geita.
Mpango huo unatekelezwa kupitia mradi wa usambazaji wa taulo za kike kwa wanafunzi waweze kujisitiri wakati wa hedhi pamoja na ufadhili wa mafunzo ya afya ya uzazi kwa walimu walezi.
Ofisa Uhusiano kutoka GGML, Doreen Denice ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geita na kueleza dhamira ni kupunguza tatizo la mdondoko wa wanafunzi hususani jinsia ya kike.
Anesema shule zinazonufaika moja kwa moja na mpango huo ni zile zinazozunguka mgodi wa GGML kwa halmashauri zote mbili, ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Halmshauri ya Manispaa ya Geita.
“Mwaka huu tumetoa taulo za kike zaidi ya 80,000 na tumezitoa kwenye shule 57 zinazunguka mgodi wa GGML, lengo ni kusaidia watoto wa kike waweze kusoma vizuri, na kutimiza malengo yao.
“Mpango huu ni endelevu tumekuwa tukifanya hivi kwa miaka yote, na tutaendelea kushirikiana na halmashauri zote mbili ili tuweze kuona tunawasaidiaje watoto wa kike na wa kiume kwa pamoja,” amesema.
Doreen amesema jumla ya walimu walezi 126 kati yao walimu 59 wa Manispaa ya Geita na walimu 67 wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wamepatiwa mafunzo ya afya ya uzazi na hedhi salama kwa mwaka 2025.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Rehema Mustapha amesema mpango huo wa GGML utawaweka salama wanafunzi na kuwalinda dhidi ya mazingira hatarishi ya afya ya uzazi.
“Kupitia mafunzo haya ya uzazi salama, wanafunzi wanaelewa madhara ya kujiingiza kwenye ngono wakiwa wadogo, kwa hiyo wanaweza kujiepusha na kufikia malengo yao na pia kujilinda wakati wa hedhi,” amesema.
Rehema amesema walimu walezi waliopata mafunzo ya elimu ya afya ya uzazi na hedhi salama watakuwa mabalozi kwenye shule zao ili kufanikisha elimu hiyo iwafikie, siyo tu wanafunzi bali pia walimu wengine waliopo shuleni.
Mwalimu Mkuu shule ya msingi Nyakabale, Veronica Samo amesema changamoto za kiuchumi zimefanya wasichana wengi kushindwa kununua taulo za kike na kufanya mahudhurio yao yawe ya kusuasua.