Elimu ya unyonyeshaji yazaa matunda

Habari Leo
Published: Jul 30, 2025 11:46:41 EAT   |  Educational

DAR-ES-SALAAM : VIWANGO vya unyonyeshaji wa maziwa ya mama nchini Tanzania vinaendelea kuimarika, huku asilimia ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee ikiongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 64 mwaka 2022.

DAR-ES-SALAAM : VIWANGO vya unyonyeshaji wa maziwa ya mama nchini Tanzania vinaendelea kuimarika, huku asilimia ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee ikiongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 64 mwaka 2022.

Kadhalika, watoto wanaonyonyeshwa ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa wameongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 70 mwaka 2022, hatua inayotajwa kuwa na mchango mkubwa katika afya na maendeleo ya mtoto.

Takwimu hizo zilitolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe, wakati wa uzinduzi wa wiki ya Unyonyeshaji wa maziwa ya Mama Duniani, ambapo pia amezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Kuzuia na Kutibu Ukondefu na Uvimbe utokanao na Ukondefu Mkali (Nutritional Oedema).

Kwa niaba ya Dk. Shekalaghe, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Afya), Prof. Tumaini Nagu, amesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto ya watoto wachache kuendelea kunyonya hadi umri unaoshauriwa. “Kwa sasa ni asilimia 35 tu ya watoto wenye umri wa miezi 20 hadi 24 wanaoendelea kunyonya, hali inayohatarisha mahitaji ya lishe bora kwa watoto hao,” amesema Prof. Nagu.

Ameongeza kuwa kutonyonyesha kikamilifu ni miongoni mwa sababu kuu za utapiamlo na ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2022 zinaonesha kuwa watoto milioni 45 duniani, sawa na asilimia 6.8, wanakabiliwa na ukondefu, huku asilimia 2.1 wakikabiliwa na ukondefu mkali.

Hata hivyo, Prof. Nagu ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua, kwani kiwango cha ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano kimepungua hadi kufikia asilimia 3, chini ya kiwango cha juu kilichowekwa na WHO cha asilimia 5. Hii ni sawa na watoto 620,000 kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022. Amesema hatua hiyo imesaidiwa na uwepo wa mwongozo wa usimamizi wa matibabu ya utapiamlo mkali (IMAM 2018), ambao umeendelea kuhuishwa ili kuendana na ushahidi wa kisayansi na hali halisi ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Action Against Hunger Tanzania, Zachary Imeje, amesema uzinduzi wa mwongozo mpya wa mwaka 2025 ni hatua muhimu inayolenga kubadilisha mitazamo ya jamii kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji. “Tunaamini mwongozo huu mpya ni ahadi ya kitaifa ya kuwafikia watoto walio hatarini kwa huduma bora na kwa wakati. Unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni haki ya mtoto na jukumu la jamii yote,” amesema Imeje.

Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji yanatarajiwa kuleta msukumo mpya katika jitihada za kupunguza utapiamlo na kuhakikisha watoto wote wanapata lishe bora kuanzia siku ya kwanza ya maisha yao. SOMA: Asilimia 40 ya watoto hawanyonyeshwi