Dk Samia aandika historia DUCE

Ni wazi sasa — historia ya elimu ya juu nchini Tanzania inaandikwa upya katika ardhi ya Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE). Wakati majengo makubwa yakipanda kama ishara ya matumaini mapya, hewa ya mageuzi inahisiwa kila kona ya chuo hicho, shukrani kwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk …
The post Dk Samia aandika historia DUCE first appeared on HabariLeo.
Ni wazi sasa — historia ya elimu ya juu nchini Tanzania inaandikwa upya katika ardhi ya Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Wakati majengo makubwa yakipanda kama ishara ya matumaini mapya, hewa ya mageuzi inahisiwa kila kona ya chuo hicho, shukrani kwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
Kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET), DUCE imepata uwekezaji mkubwa zaidi tangu lilipoanzishwa mwaka 2005 — kiasi cha dola za Kimarekani milioni nane, sawa na zaidi ya Sh Bilioni 19, ambazo zimeleta mageuzi ya kweli katika miundombinu, teknolojia na ubora wa elimu.
Rasi wa DUCE, Prof Stephen Maluka, amesema mradi wa HEET ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kubadilisha sekta ya elimu kuwa chachu ya maendeleo ya taifa.
“Huu ni uwekezaji mkubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa DUCE. Ni uthibitisho kwamba Serikali ya Dk Samia imeamua kuwekeza nguvu katika elimu bora na tafiti zenye matokeo. Sisi DUCE tumejipanga kuhakikisha tunakuwa mfano wa usimamizi wa miradi ya maendeleo,” amesema Prof Maluka.
Chini ya mradi huo, amesema majengo mawili makubwa yanaendelea kujengwa — Jengo la Shahada za Uzamili na Jengo la Kitivo cha Sanaa na Sayansi Jamii.
Majengo hayo yatakuwa na maabara za kisasa, kumbi za mihadhara, ofisi za watumishi, na miundombinu ya elimu maalumu, hatua itakayoongeza uwezo wa DUCE kutoa elimu ya ushindani wa kimataifa.
Lakini si majengo pekee yanayobadilika — maktaba ya DUCE imeingia zama za kidigitali na kwamba kwa kupitia HEET, amesema wanafunzi na wahadhiri sasa wanaweza kupata huduma za maktaba popote na muda wowote bila ulazima wa kufika chuoni.
“Hii ni hatua kubwa kuelekea elimu mtandaoni (e-learning) ambayo inapanua wigo wa upatikanaji wa maarifa,” amesema Prof Maluka.
Amesema mabadiliko makubwa pia yameonekana katika matumizi ya TEHAMA kwa kuongeza kasi ya mtandao kutoka Mbps 200 hadi 600, huku mkongo wa ndani wa intaneti ukikarabatiwa na kusimika mfumo wa Masijala Mtandao (e-registry) ambao umeondoa urasimu na matumizi ya makaratasi.
Amesema wahadhiri pia wamepewa mafunzo maalum ya kufundisha kwa kutumia majukwaa ya kidigitali.
“Mradi wa HEET si tu unajenga majengo — unajenga mustakabali wa taifa,” anasema.
Naye Naibu Rasi, Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof Amani Lusekelo, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha wanataaluma 16 wa DUCE kusomea Shahada za Umahiri na Uzamivu (Masters na PhDs) katika vyuo vikuu mashuhuri duniani kama Aberdeen (Scotland), Bielefeld (Ujerumani), Brunel (Uingereza) na University of Zululand (Afrika Kusini).
“Wengi wao wamerudi na sasa wanatumia ujuzi huo kuboresha mitaala, tafiti na mbinu za ufundishaji. Hii ni sehemu ya mageuzi ya kimfumo yanayoendelea DUCE,” amesema Prof Lusekelo.
Kwa upande wake, Naibu Rasi, Mipango, Fedha na Utawala, Prof Pendo Malangwa, amesema HEET pia imeboresha vyumba vya mihadhara, hosteli na ofisi kwa kuzipatia kompyuta, viti na meza mpya, hivyo kuimarisha mazingira ya ujifunzaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shahada za Awali, Dk Joel Kayombo, amesema mradi huo umeleta mageuzi katika mitaala ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Tulifanya utafiti maalum wa kufuatilia wahitimu (tracer study) ili kubaini changamoto na mafanikio. Sasa mitaala yetu inazalisha wahitimu wanaotatua matatizo halisi ya jamii,” amesema.
Amesema DUCE imegeuka kuwa mfano wa namna Serikali inavyoweza kuunganisha rasilimali, teknolojia na maono katika kuijenga Tanzania ya elimu bora.
The post Dk Samia aandika historia DUCE first appeared on HabariLeo.