Dk Kijaji: Mashindano makubwa gofu Afrika kufanyika Serengeti
MARA; Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amesema Uwanja wa Gofu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti utawezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya gofu ya Afrika na kimataifa, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya watalii, mapato na kuitangaza nchi kupitia utalii wa michezo. Akizungumza leo Oktoba 18, 2026, wakati wa uzinduzi wa …
MARA; Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amesema Uwanja wa Gofu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti utawezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya gofu ya Afrika na kimataifa, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya watalii, mapato na kuitangaza nchi kupitia utalii wa michezo.
Akizungumza leo Oktoba 18, 2026, wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa Gofu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, uliofanyika Fort Ikoma, Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara, Dk Kijaji aliyemwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan, amesema ujenzi wa uwanja huo ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa wanyamapori na utalii wa michezo barani Afrika.
Amesema gofu ni miongoni mwa michezo inayoweza kuvutia watalii wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuongeza mapato yatokanayo na utalii.
“Kupitia uwanja huu tunatarajia kuongeza mapato ya utalii, kuvutia watalii,, kuongeza muda wa wageni kukaa nchini, kuchochea uwekezaji katika hoteli na huduma nyingine pamoja na kutengeneza ajira mpya kwa vijana na kuongeza mchango wa utalii katika uchumi wa taifa,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa kuanzisha programu za mafunzo ya gofu kwa vijana, hususan wanafunzi wa shule zinazozunguka eneo hilo la uwanja , ili kuwajengea uwezo na kukuza vipaji vitakavyoweza kuwakilisha nchi katika mashindano ya kitaifa na kimataifa siku zijazo.
Amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kutekeleza maono ya Rais kwa kuanzisha aina mpya ya utalii inayounganisha uhifadhi wa maliasili na michezo.
Pia aliipongeza Bodi ya TANAPA pamoja na wajumbe wake kwa kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Rais hadi kufikia hatua ya uzinduzi wa uwanja huo.
Aidha ameielekeza TANAPA kuandaa mpango mkakati utakaohakikisha uwanja huo unaendeshwa kwa uendelevu kuleta manufaa
Naye Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa, alisema ujenzi wa Uwanja wa Gofu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti umegharimu Sh bilioni 8.5.
Mwishawa amesema uwanja huo una barabara ya mzunguko yenye urefu wa kilomita 5.2, huduma ya umeme wa uhakika kutoka gridi ya taifa, jengo la klabu ya gofu, maeneo ya mazoezi pamoja na vifaa muhimu kwa ajili ya uendeshaji .
Rais wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Gilman Kasiga, ameishukuru TANAPA kwa kujenga uwanja huo na kusema chama hicho kitaendelea kushirikiana na shirika hilo katika kuendeleza mchezo wa gofu nchini.