Dira 2050 yataja sekta za mageuzi kiuchumi

Habari Leo
Published: Jul 24, 2025 07:43:59 EAT   |  Travel

DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050 imetaja sekta zenye fursa ya mageuzi kiuchumi ikiwemo ya viwanda, kilimo na utalii. Imeeleza kuwa Tanzania inalenga kuwa kitovu cha viwanda chenye ushindani kimataifa ifikapo mwaka 2050 ikitumia ongezeko la idadi ya watu, maendeleo ya kiteknolojia na msingi wake imara wa kilimo, kama nyenzo muhimu. “Ili kufanikisha azma hii, …

DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050 imetaja sekta zenye fursa ya mageuzi kiuchumi ikiwemo ya viwanda, kilimo na utalii.

Imeeleza kuwa Tanzania inalenga kuwa kitovu cha viwanda chenye ushindani kimataifa ifikapo mwaka 2050 ikitumia ongezeko la idadi ya watu, maendeleo ya kiteknolojia na msingi wake imara wa kilimo, kama nyenzo muhimu.

“Ili kufanikisha azma hii, ni muhimu kuimarisha miundombinu, kuboresha mazingira wezeshi ya biashara, kuimarisha sera, kujenga ujuzi wa rasilimali watu na kupanua wigo wa upatikanaji wa mitaji,” imeeleza.

Dira 2050 inaeleza kwa sasa sekta ya viwanda inachangia asilimia 8.1 ya pato la Taifa na inakua kwa asilimia 8 kwa mwaka.

Imeeleza sekta hiyo ina uwezo mkubwa wa kuwa na athari chanya katika sekta nyingine kama vile usindikaji wa mazao na uzalishaji wa vifaa vya ujenzi.

“Hii itaongeza thamani ya ndani, itapunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuboresha uzalishaji wa mauzo ya nje,” imeeleza.

Kilimo Dira 2050 imeeleza hadi mwaka 2050 sekta ya kilimo inatarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa yenye tija, endelevu na yenye ushindani wa hali ya juu.

“Hii itaifanya Tanzania kuwa kitovu cha chakula katika ukanda wa Afrika. Ili kufanikisha hili, kilimo cha Tanzania kitalazimika kuhama kutoka mazao ya asili ya nafaka kwenda kwenye mazao mbadala yenye thamani ya juu,” imeeleza.

Dira imeeleza utahitajika uwekezaji mkubwa katika teknolojia ya kisasa, miundombinu mahususi ya kukabili tabianchi na kukuza biashara za kilimo na mikakati ya kuwasaidia wakulima.

“Aidha, matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kilimo yatawaunganisha wakulima na masoko, kukuza ufanisi na kuleta faida. Itakuwa muhimu vilevile kuwekeza katika nishati nafuu, upatikanaji bora wa fedha, upanuzi wa mitandao ya masoko, na kuhimiza mbinu endelevu za kilimo,” imeeleza.

Kwa mujibu wa Dira 2050 sekta ya kilimo bado ni mhimili wa uchumi wa Tanzania ikichangia asilimia 26.5 ya pato la Taifa, ikiajiri asilimia 65 ya nguvukazi na kuzalisha asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje.

“Sekta hii ina uwezo wa kuzalisha ajira nyingi na kuchochea ongezeko la mapato kupitia mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani,” imeeleza Dira 2050. Imeongeza: “Uhusiano wake na sekta za viwanda, usafirishaji, na biashara unabainisha nafasi yake katika kukuza ajira na uchumi. Katika siku zijazo, kilimo bado kitaendelea kuwa nguzo ya uchumi wa Tanzania”.

Utalii Dira 2050 imeeleza hadi kufikia mwaka 2050 utalii unatarajiwa kuwa moja ya vyanzo vikuu vya ajira za moja kwa moja na zinginezo.

Imeeleza sekta hiyo itapanuka zaidi na kuvutia wageni wa nje na ndani kupitia utalii unaohusisha utamaduni, urithi wa asili na malikale, utalii endelevu wa mazingira, utalii wa meli na fukwe, utalii wa uwindaji na wa mikutano na maonesho hivyo kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

“Ukuaji huu utategemea uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu, utangazaji katika masoko lengwa, na ushirikishwaji wa jamii katika maeneo mbalimbali ya utalii,” imeeleza Dira 2050.

Imeongeza: “Ni muhimu kukuza utamaduni wa kutoa huduma bora ili kuimarisha ushindani wa utalii wa Tanzania. Kupitia hatua hizi, Tanzania inalenga kuwa kitovu cha utalii barani Afrika ifikapo mwaka 2050.”