Chalamila: Usafi si wa kusubiri kukumbushwa

Habari Leo
Published: Sep 29, 2026 09:49:13 EAT   |  News

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka viongozi katika maeneo mbalimbali kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Serikali, hususan kuhusu usafi na utunzaji wa mazingira, akisisitiza kuwa hawapaswi kusubiri kukumbushwa mara kwa mara kuhusu wajibu wao. Chalamila ametoa kauli hiyo leo wakati wa ziara yake Wilaya ya Kinondoni, ambapo alitembelea …

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka viongozi katika maeneo mbalimbali kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Serikali, hususan kuhusu usafi na utunzaji wa mazingira, akisisitiza kuwa hawapaswi kusubiri kukumbushwa mara kwa mara kuhusu wajibu wao.

Chalamila ametoa kauli hiyo leo wakati wa ziara yake Wilaya ya Kinondoni, ambapo alitembelea Daraja la Mkwajuni na Mto Ng’ombe kukagua hatua zilizochukuliwa kukabiliana na mvua za El Niño.

Amesema Manispaa ya Kinondoni imefanya kazi nzuri katika kutekeleza maelekezo ya Makamu wa Rais kuhusu usafi na utunzaji wa mazingira, hatua inayopaswa kuigwa na maeneo mengine.

Amesema kukumbushwa mara moja na viongozi si kosa, lakini si jambo zuri kwa kiongozi kuendelea kukumbushwa mara kwa mara kuhusu majukumu yake, hivyo amewataka viongozi kuongeza kasi katika usimamizi na utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na Serikali.

Aidha, amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa kusimamia kwa karibu maeneo yao na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi, huku akisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika kulinda mazingira.

Chalamila amesema kasi ya ukuaji wa Dar es Salaam inapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya tabia za wananchi katika utunzaji wa mazingira, akieleza kuwa maeneo ambayo miaka michache iliyopita hayakuwa na majengo mengi sasa yameendelea kujengwa kutokana na ongezeko la shughuli za maendeleo.

Amesema hali hiyo inahitaji wananchi kujipanga na kutambua kuwa wanaishi katika jiji linalokua kwa kasi, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto za mazingira, huku akiwataka kuwa sehemu ya suluhisho kwa kushiriki kikamilifu katika usafi na utunzaji wa maeneo yao.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Warda Obathany, amesema wilaya hiyo imejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kutupa taka kwenye mitaro, ikiwemo kuziba kwa mifereji na kusababisha kero kwa wakazi.

Amesema elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kuhakikisha mifereji inakuwa katika hali inayowezesha maji kupita kwa urahisi wakati wa mvua.