Bunifu MUHAS suluhisho za changamoto za afya

Habari Leo
Published: Aug 20, 2026 19:28:41 EAT   |  Educational

TANGA: Ubunifu wa wanafunzi na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) umeendelea kuibua matumaini kwa wananchi katika kutafuta suluhisho za changamoto mbalimbali za afya zinazowakabili katika maisha ya kila siku. Kupitia banda la MUHAS katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayofanyika katika Shule ya Sekondari Usagara, wananchi …

TANGA: Ubunifu wa wanafunzi na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) umeendelea kuibua matumaini kwa wananchi katika kutafuta suluhisho za changamoto mbalimbali za afya zinazowakabili katika maisha ya kila siku.

Kupitia banda la MUHAS katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayofanyika katika Shule ya Sekondari Usagara, wananchi na wanafunzi wanapata nafasi ya kujionea bunifu zinazolenga kuboresha huduma za afya na kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma muhimu.

Miongoni mwa bunifu zinazooneshwa ni MoyoGuard, BiliMeasure, Siku Smart, Biosafe, Robospine, QR Dharura na Bridging Silence, ambazo zimeibua hamasa miongoni mwa wageni kutokana na kulenga changamoto zinazogusa maisha ya wananchi.

Maonesho hayo pia yamekuwa darasa kwa wanafunzi wanaotembelea banda hilo, ambapo wanapata fursa ya kuona kwa vitendo namna maarifa wanayopata shuleni na vyuoni yanavyoweza kubadilishwa kuwa bidhaa au teknolojia yenye manufaa kwa jamii.

Kwa wananchi, ubunifu huo unaonesha umuhimu wa kuwekeza katika vijana na kuwapa mazingira bora ya kutumia vipaji, elimu na teknolojia kutengeneza majibu ya changamoto zinazowazunguka.

Wiki hiyo inaendelea hadi Agosti 24, 2026, ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii, hususan vijana, kutambua nafasi ya elimu, ujuzi na ubunifu katika kujenga jamii yenye uwezo wa kujitegemea na kutatua changamoto zake.