Barabara Kinyanambo Madibira yageuka kisu cha mgongoni kwa Kigahe

IRINGA: Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Mufindi Kaskazini wamemkaba kwa maswali Mbunge anayemaliza muda wake, Exaud Kigahe, wakitaka majibu ya kwanini barabara ya Kinyanambo–Madibira, iliyoahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami tangu mwaka 2016, hadi leo haijakamilika, huku akiomba tena ridhaa ya kuwaongoza kwa ahadi ile ile. Katika kikao cha kampeni kilichofanyika …
IRINGA: Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Mufindi Kaskazini wamemkaba kwa maswali Mbunge anayemaliza muda wake, Exaud Kigahe, wakitaka majibu ya kwanini barabara ya Kinyanambo–Madibira, iliyoahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami tangu mwaka 2016, hadi leo haijakamilika, huku akiomba tena ridhaa ya kuwaongoza kwa ahadi ile ile.
Katika kikao cha kampeni kilichofanyika Kata ya Igombavanu na Sadani wanachama walimtaka Kigahe kueleza sababu za kushindwa kutekeleza ahadi hiyo katika miaka yake mitano bungeni, licha ya kuishika pia nafasi ya Naibu Waziri.
“Ulikuwepo madarakani miaka mitano, barabara hiyo mliifanya ya kuombea kura na hakuna utekelezaji. Leo unataka tena, tukuamini vipi?” alihoji mmoja wa wanachama.
Akijibu, Kigahe alisema ujenzi wa barabara hiyo umeanza kwa kipande cha kilomita 25, na kwamba imeshaingizwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 kwa hatua za uendelezaji.
“Maendeleo ni hatua. Tumepata lami kwenye baadhi ya barabara za jimbo, na Kinyanambo nayo tumeanza,” alisema, akiongeza kuwa vifaa na mitambo ya ujenzi vinaendelea na kazi Mafinga.
Mbali na suala la barabara, Kigahe alibanwa kuhusu miradi mingine ikiwemo chuo cha VETA kilichohamishiwa Nyololo, mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu, na mradi wa maji Sadani Kihata.
Akijibu swali la chuo cha VETA, Kigahe alisema maamuzi hayo ni ya serikali na si mtu mmoja, na kwamba eneo lililoachwa litaendelezwa kwa mradi mwingine kama chuo au kiwanda.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10, alidai ilisitiswa kutokana na kuwepo kwa matumizi hewa na vikundi vya uongo, lakini utaratibu mpya umeandaliwa ili vikundi vya kijasiriamali vipate fedha na kurejesha.
Aidha, alikanusha tuhuma za kuondoa mradi wa maji Sadani Kihata, akisema uliahirishwa ili kutoa kipaumbele kwa mradi mkubwa wa maji wa Sh bilioni 42 utakaonufaisha tarafa nzima ya Sadani.
Kwenye mkutano huo, wagombea wengine wa CCM walitumia nafasi hiyo kuwasilisha sera na ahadi zao.
Alban Lutambi aliahidi kutumia uzoefu wake wa miaka 15 kwenye sekta ya barabara kukuza uchumi wa kilimo na kutoa ajira kwa vijana kupitia upatikanaji wa pembejeo kwa tija.
Prof. Obadia Nyongole aliahidi kusimamia barabara ya Kinyanambo–Madibira, kuongeza huduma za madaktari bingwa kila mwaka katika Hospitali ya Sadani, na kuimarisha huduma kwa akinamama wajawazito.
Lucman Melabu, kwa upande wake, aliahidi kushughulikia sekta za barabara, afya na pembejeo, akitumia taswira ya “kumuua panya nyumbani” kama mfano wa kumaliza changamoto zinazoikabili Mufindi Kaskazini.